<p>Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini amewataka makatibu tawala wa wilaya na Maofisa Ustawi wa Jamii&nbsp; katika halmashauri&nbsp; zote za mikoa ya&nbsp; Mara, Mwanza, Kagera, Geita,Simiyu na Shinyanga kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuandika na kuhifadhi wosia, kusajili vizazi, vifo ,ndoa&nbsp; na taraka ili&nbsp; &nbsp;kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi zitakazo saidia&nbsp; kupanga mipango ya maendeleo pamoja na kuepusha migogoro ya mirathi katika jamii.</p><p>Akizungumza katika kijiji cha kyabakari wilayani Butiama Mkoani Mara wakati wa kufungua mafunzo hayo kuhusu huduma zinazotolewa na wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa wadau wa usajili katika mikoa hiyo, Naibu Waziri Sagini amesema mafunzo hayo yataleta mabadiliko makubwa kwa kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.</p><p>Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi&nbsp; &nbsp;amesema Wakala imekuwa ikiandaa mafunzo na vikao na wadau wa makundi mbalimbali kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kujadiliana namna bora ya&nbsp; kuongeza ufanisi pamoja na kukumbushana wajibu na majukumu ya kila mmoja ili kusaidia katika kutoa huduma bora kwa wananchi.</p><p>Naye Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Moses Kaegele amesema kwa kuwa Serikali haina dini ingawa watu wake ni waumini wa Imani mbalimbali hivyo wote wataheshimiwa na kuthaminiwa kwa usawa na kuungana na kushikamana kama jamii moja katika kufuata misingi ya sheria taratibu na miongozo ya nchi yetu.</p>